YESU ANAWEZA KUKUTOA KATIKA SHIDA ULIYONAYO, AMINI TU!

My photo
We're delightly to preach the word of almighty God

Wednesday, April 26, 2017

Sehemu ya pili ya somo letu lenye kichwa kiitwacho "NAMNA YA KUJITOA KATIKA HISTORIA YAKO YA NYUMA


 MAANA YA HISTORIA
    Ninapo zungumza kwa habari ya historia, ninakuwa ninazungumzia jumla ya namna ambavyo mtu ameishi na watu, na kufanya vitu ambavyo vikajenga kumbukumbu katika maisha yake, pamoja kwamba huyo mtu anaweza akasahau au akakumbuka, kumbukumbu hiyo pia yaweza kuwa njema au siyo njema machoni kwa watu au kwa mtu yule (yaani mhusika). Na siku zote vile vitu vizuri vinaweza vikasahaulika kwa haraka zaidi  lakini vile vitu vibaya inakuwa ni vigumu kusahaulika kwa sababu vinaumiza mioyo ya watu na kutia doa, na mara nyingi doa hilo likitazamwa na moyo huonekana na kuleta kumbukumbu ya kisababishi cha doa hilo. Mfano mzuri ni pale tunapomuona mtu alikuwa ni kiongozi mzuri tu, lakini baadaye akafanya jambo baya, huwa anakuja kuonekana kuwa ni mtu mbaya na kosa hilo hufunika mazuri yote ambayo amewahi kuyafanya.
   Vitu vyote na shughuli zote ambazo mtu amezipitia kabla ya kufika hapo alipo, tunapo muona leo. Tunaona kwenye misiba mbali mabali, historia ya marehemu inasomwa, wataeleza mambo mengi aliyoyafanya, kama alisoma wataeleza alisoma wapi, watasema sababu ya kifo chake, watasema kaacha watoto wangapi (kama alikuwa na familia) na mengineyo mengi kulingana na utaratibu utakao wekwa. Yako mambo mengi mtu anayokuwa ameyafanya ambayo wakati wa uhai wake hatuwezi kuyafahamu lakini baada ya kifo chake vitu huwa vinakuwa wazi kabisa.
    Na historia hubadilika, kwa kuwa tabia ni jumla ya mwenendo wa maisha ya mtu, na tabia ndiyo inayojenga historia ya mtu. Unapozungumza kuhusu historia bila kuzungumzia tabia, ni sawa na kungoja meli uwanja wa ndege. Maana yake ni kwamba, tabia ni kama matofari wakati wa kujenga nyumba, historia ni jumla ya tabia zote ambazo mtu anakuwa amezionyesha kwa kipindi Fulani. Huwezi kusema huyu mtu ana historia mbaya kama umemuona mara moja tu akifanya kitu Fulani kibaya (japo pia inawezekana, kwa sababu jambo hilo linaingia katika historia ya maisha yake), lakini tukizungumza kwa hali ya kawaida, historia ya mtu inabidi ipimwe kwa muda fulani, na ndiyo maana historia inajengwa na tabia mbali mbali, nzuri au mbaya,zote kwa pamoja zinajenga historia ya mtu.
Viko vitu ambavyo vinaweza kuchangia kubadilika kwa tabia na mwenendo (historia) wa mtu;
i) Kitu cha kwanza ni “Msukumo wa ndani ambao kila mtu kazaliwa nao”. Huu ni msukumo ambao ni wa ndani ambao ni wa asili ambao ukija ni lazima uutimize, mfano; Mtu anapata msukumo wa kula (njaa), hapa suluhisho ni moja tu, ambalo ni kula, na siyo kwamba wewe ndo unauleta msukumo huo. Lakini lazima uwe na uwezo wa kuweza kuuthibiti msukumo huo pamoja kwamba ni lazima uutimize.
ii) “Nguvu ya akili”. Akili ni uelewa ambao anakuwa nao mtu, ambao unamsaidia aweze kujitambua, ambao pia unamsaidia akumbuke na ni chanzo cha mawazo ya mtu. Hapa mtu anatumia uelewa wake kwa kujipima kama anastahiri kufanya kitu Fulani, na kama anatakiwa afanye kitu Fulani, je! Afanye kwa wakati upi?, pia mtu hapa anaangalia madhara yay eye kuweza kufanya kitu Fulani, ni kweli kwamba huu ni msukumo wa ndani ambao kwa hali ya kawaida ni lazima ni fanye, lakini je! Ni lazima nifanye? Na kama ni lazima nifanye,je! Ni lazima nifanye kwa wakati huu? Nikifanya jamii itanitazama vipi? Je! thamani yangu itashuka kwa jamii ninayoishi? Kama inatakiwa nifanye,je! Nilazima nifanye kwa mtindo huu?. Hapa mtu anjitathmini kufanya kitu Fulani ambacho kinasababishwa na msukumo wa ndani, lakini yeye anajaribu kutazama thamani yake katika jamii, kwamba je! Kile kitu kinakubalika katika jamii anayoiishi?. Jambo hili la pili ninaweza nikasema ni la mhimu sana kwa sababu linakitazama kitu kabla hujakifanya, linakitathmini kulingana na sheria na taratibu ambavyo zinavyohitaji na kutoa tafsiri ya kile kitu, ili mtu aepukane na aibu na kuvunjika kwa heshima yake katika jamii.
iii) Nguvu kuu, hii ni nguvu ambayo ndani yake imebeba akili, ambayo kwa kawaida inajitegemea, na kuweka bayana uelewa na uhalisi wa mambo. Hii ni nguvu ambayo inuwezo wa kuthibiti “nguvu ya msukumo wa ndani” na nguvu ya akili. Hii inakagua na kutazama vile vitu ambavyo mtu kavifanya, je! Ni sahihi kufanywa, na kama ni sahihi, je! Ni kwa namna ilivyotakiwa kufanywa? Na je! Ni kwa wakati ambao vilitakiwa kufanywa?. Hii nguvu inawakilisha jukumu la wazazi, sharia na taratibu za nchi, sharia na taratibu za kidini. Lakini kwetu sisi, hii nguvu ni ile sharia na taratibu ambazo Mungu kaziweka kwetu sisi. Na kushindwa kuzingatia sharia hii ni sawa na kuandaa bomu ambalo litakulipua wewe mwenyewe. Vitu vyote vile viwili vya mwanzo vinaweza vikashindwa lakini kitu hiki cha mwisho ni cha muhimu na cha msingi sana katika maisha yako wewe kama mkristo. Rumi 7:23-25
     Historia inajengwa na vitu vyote hivyo vitatu vilivyotajwa hapo juu, na historia yako kuwa mbaya au nzuri inategemea sana jinsi ambavyo hivyo vitu vitatu umevitazama vipi na umeviweka vipi katika maisha yako, ni kweli kabisa kuwa ni vigumu kuweza kuepuka vitu vingine, lakini  inawezekana maana palipo na nia pana njia; Wafilipi 4:13. Historia yako itakuwa njema nay a kuigwa kama hutatumia akili zako wewe mwenyewe, maana peke yako hutaweza. Wako watu wao huwa wanasema huwezi kuwa mtakatifu ukiwa duniani, mimi ninapingana nao vikali kabisa; Zaburi 16:3, hana maana kwamba watakatifu walioko mbinguni hawathamini, ni kwa sababu tu kuwa hawa watakatifu walioko duniani wamekuwa ni watakatifu, licha ya kuwa wanaishi katika ulimwengu wa dhambi lakini wamekuwa ni watakatifu.
Ukisoma habari ya mfalme Hezekia, Isaya 38:1-8, anatokewa na nabii Isaya mwana wa Amozi kwa habari ya ugonjwa wake, anaambiwa Hezekia hutapona bali utakufa; Hezekia “akasema, Ee BWANA, kumbuka haya”, huwezi kumwambia mtu akumbuke kama hukumaanisha kuwa aangalie vitu au kitu ambacho ni muhimu ambacho umewahi kukifanya katika maisha yako ambacho kikitazamwa kinaleta maana kubwa wakati huo. Yako mambo aliyoyafanya mfalme Hezekia, yakajenga historia ya maisha yake ambayo Mungu akiyatazama anaona kweli huyu mtu kakamilika. Yako mambo makubwa aliyafanya Hezekia na Biblia inamsifu inasema hakuna mfalme aliyekuwa mzuri kabla na baada yake , 2Nyakati 18:1-8.
Jinsi ambavyo unaweza ukaishi leo ndivyo ambavyo unakuwa unaiandaa kesho yako. Vile alivyoishi mfalme Hezekia ndivyo alivyompendeza Mungu, ndiyo maana tunamuona mfalme Hezekia anpata neema kuu tatu machoni mwa Mungu;
i) Kujua wakati wake wa kufa. Kupewa taarifa kuwa atakufa wakati huu.
ii) Kushauriwa kitu cha kufanya, maana aliambiwa hatapona bali atakufa, hivyo atengeneze mambo ya nyumba yake. Na ushauri mzuri ni ule atakao kupa Mungu, maana anakuwa na uhakika nao, lakini unakuwa ni uhakika wa kweli.
iii) Kuongezewa miaka ya uhai wake. Baada ya mfalme Hezekia kupewa taarifa kuwa atakufa wala hatadumu, alichokifanya hakung’ang’ana na nabii Isaya, bali aligeuza uso wake kwenye ukuta na kumwita Mungu na akamwambia akumbuke jinsi alivyoenenda kwa ukamilifu mbele zake.
   Hii ni heshima kubwa kati ya heshima ambazo Mungu amewahi kuzionyesha kwa mwanadamu, Hezekia alipata heshima kubwa na upendeleo mkubwa sana, yaani kule kupewa taarifa tu kuwa aandae mambo ya nyumba yake maana atakufa wala hatapona; ni neema kubwa mno, ni watu wangapi wamewahi kupata neema hiyo?Kwa watu wa leo wangesema ya kuwa basi kwa kuwa amesema nitakufa ngoja nimalizie raha na niombe msamaha ili nife katika maisha matakatifu. Wapo watu wanakufa na baadae ndugu zao wanakwenda kuwaombea makanisani ili wapate rehema, wanasahau neno la Mungu linasemaje katika neno lake; Waebrania 9:27. Kila mtu atabeba mzigo wake yeye mwenyewe, atawjibika kwa kile alichokifanya akiwa hapa duniani, historia yako imebeba maana kubwa na kuonyeshs njia unayopaswa kuingia.
Mungu akutunze, tukutane hapo kesho,by Ev.Dr Ayubu Mathias Kwandikwa

No comments:

Post a Comment